MASOMO YA MISA, MACHI 22, 2022: JUMATANO, JUMA LA 3 LA KWARESIMA
Welcome Back.
Updated at: 2024-05-27 07:09:45 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Musa aliwaambia makutano: Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mmzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwmingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi,5 mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia⁵ amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,Amewabariki wanao ndani yako. (K)
Huipeleka amri yake juu ya nchi,Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)
Humhubiri Yakobo neno lake,Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)
Mbegu neno la Mungu, mpanzi lakini ni Kristu; Yeyote ampataye, ataishi milele.
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:49 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Yer. 18-18-20
Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.
Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili nisema mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Zab. 31:4-5, 13-15 (K) 16
(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.
Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote.
Waliposhauriana juu yangu,
Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)
Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
Lk. 8:15
Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.
Mt. 20:17-28
Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.
Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywa kikombe change; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.
Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:50 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Alikuja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.
1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. (K)
Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
2. Macho ya watu yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. (K)
3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
Aleluya Aleluya!
Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Aleluya
Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.
Neno la Bwana..... Sifa Kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:44 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2022
IJUMAA, JUMA LA 3 LA KWARESIMA
Isa. 7:10 – 14
Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Zab. 40:6 – 10 (K) 7 , 8
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
Katika gombo la chuo nimeandikiwa
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)
Ebr. 10:4 – 10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Mungu.
Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
Yn. 1:14
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukaona utukufu wake.
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:40 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari, na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko.
Na ulimi wetu kelele za furaha. (K)
Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa Imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa Imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yoyote kuifikia kiyama ya wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.
Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, kwa maana ni mwenye neema na huruma.
Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha.
Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hili wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki.
Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.
Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.
Updated at: 2024-05-27 07:09:34 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Wote wanionao hunicheka sana
Hinifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
Husema: Umtegemee Bwana; na amponye;
Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. (K)
Kwa maana mbwa wamenizunguka;
Kusanyiko la waovu wamenisonga;
Yamenizua mikono na miguu.
Naweza kuihesabu mifupa yangu yote. (K)
Wanagawanya nguo zangu,
Na vazi langu wanalipigia kura.
Nawe, Bwana, usiwe mbali,
Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. (K)
Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
Ninyi mnaomcha Bwana msifuni
Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni. (K)
Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
Kristu alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina.
Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.
Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka.
Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.
Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.
Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.
Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito. Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.
Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu.
Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe.
Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho.
Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.
Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi, wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo.
Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo. Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi. Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali.
Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga. Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu.
Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima; wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.
Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia? Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana. Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.
Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe. Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.
Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe. Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.
Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] Wakaketi, wakamlinda huko.
Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. Pia wale wanyang'anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.
Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.
Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo. Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu; mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe. Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi, akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi.
Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.
Updated at: 2024-05-27 07:09:23 (1 year ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo. nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.
Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana;
Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji
Katika mikono ya watu watendao maovu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Kwa ajili yako nimestahimili laumu,
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila,
Na laumu yao wanaokulaumu zimenipata. (K)
Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana,
Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu,
Katika kweli ya wokovu wako.
Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. (K)
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yetu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wake.
Mbingu na nchi zimsifu
Bahari na vyote viendavyo ndani yake. (K)
Kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia uli mwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, alive mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
Aleluya, aleluya,
Fungua mioyo yetu, ee Bwana,
Ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.
Yesu aliwaambia mitume wake: Msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum, Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.