Leo nimekuandalia Tafakari kuhusu Mambo yanayowazuia Waumini na watumishi wa Mungu Kuishi Kitakatifu na kufikia Ukamilifu. Mambo haya yanaweza yakaonekana sio dhambi au makosa kwa mtu lakini ni vikwazo kwa mtu kufikia Ukamilifu hasa anaposhindwa kuyajua na kuyaepuka. Wengi wanajiona kwamba wako salama lakini kumbe wako katika dhambi.
Updated at: 2024-06-17 17:37:01 (9 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Leo nimekuandalia Tafakari kuhusu Mambo yanayowazuia Waumini na watumishi wa Mungu Kuishi Kitakatifu na kufikia Ukamilifu. Mambo haya yanaweza yakaonekana sio dhambi au makosa kwa mtu lakini ni vikwazo kwa mtu kufikia Ukamilifu hasa anaposhindwa kuyajua na kuyaepuka. Wengi wanajiona kwamba wako salama lakini kumbe wako katika dhambi.
Mambo hayo ni kama ifuatavyo;
1. MAJIVUNO
Hii ni hali ya kujiona wa thamani sana, wakipekee na unayestahili sana.
Tofauti ya MAJIVUNO na pointi ya pili hapo chini (UMIMI) ni kwamba MAJIVUNO ni kujiona wa thamani lakini huku unatambua Yupo Mungu anayekuzidi. UMIMI ni kujiona kama Sawa na Mungu.
Kwa yale unayoyafanya: Kujiona kwamba wewe ni wa thamani na kipekee sana kwa yale uliyowahi kufanya, unayoyafanya na unayoweza kufanya. (I did, I do, I will do.)
Kwa vile Ulivyo: Kujiona kuwa wewe ni wa kipekee kwa vile ulivyo. Kusahau kuwa Vile ulivyo na vile ulivyonavyo Umepewa Bure na Mungu.
Kwa vile unavyofanyiwa: Kujiona kuwa wewe ni wa kipekee kulingana na wengine wanavyokuona na vile wanavyokufanyia.
Tafakari na ushauri kuhusu Majivuno
Unavyosoma kuwa majivuno ni hali ya kujiona wa thamani sana, wakipekee na unayestahili sana, unaweza ukafikiri sio kosa wala dhambi kujiona hivyo. Lakini makosa yanakuja kwa yale unayoyafanya kwa Majivuno hayo na kujisikia huko.
Majivuno yanakuwa dhambi pale tunapotenda kwa Majivuno na kujiona. Pale tunaposahau kwamba Upekee wetu sio kwamba tulistahili bali ni kwa Neema tuu. Tunakosea pale tunapoanza kuzarau wengine wale wasio kama sisi.
Unaweza ukafikiri kwamba hauna Majivuno lakini miongoni mwa dalili za Majivuno ni kama ifuatavyo;
1. Zarau
2. Kushindwa Kujishusha
3. Kujigamba/ Kujisifu
4. Kupenda upendeleo
5. Kujiona wa Tofauti
Ukiona kuna wakati una dalili kama hizi ujue tayari Majivuno yanajipandikiza ndani yako. Ninaposema Majivuno ni dhambi namaanisha kuwa matokeo/ matendo yanayotokana na dalili/ sifa hizi ndiyo dhambi.
Mambo ya kuzingatia kushinda Majivuno
Unyenyekevu… Unyenyekevu… Unyenyekevu ndio dawa ya Majivuno.
Utaweza kushinda majivuno kwa Kujishusha na kujiona sawa na wengine.
Unaweza ukashinda Majivuno kwa Kutambua kuwa Vile ulivyo, yale unayoweza kufanya na vile unavyofanyiwa ni Baraka za Mungu tuu. Haimaanishi kuwa umestahili sana kuwa hivyo.
Utashinda majivuno unapotambua kuwa hata wale unaowaona wako chini yako wangeweza kuwa kama wewe tuu. Ni maisha na Mipango ya Mungu ndio iliyofanya ukawa hivyo. Haimaanishi kwamba ni juhudi yako wewe. Wapo wenye Juhudi kuliko wewe lakini wapo chini yako.
2. UMIMI
Kujiona kuwa wewe ni wewe na wewe ni wa kipekee na unastahili kuliko wengine.
Tofauti kubwa na pointi ya kwanza hapo juu ni kwamba UMIMI ni Zaidi ya MAJIVUNO. Ni kujiona Hakuna wa Zaidi yako na wewe unahadhi sawa karibu na Mungu. Yaani, Mungu yupo lakini Mimi Pia nipo.
Kwa cheo, kipawa au mamlaka yako: Kujiona kwa cheo, kipawa au Mamlaka yako hakuna anayekuzidi, Mara nyingine kufikiri kwamba hata Mungu mwenyewe hawezi kukuondolea/ kukupinga. Ni kufikiri kwamba hakuna anayeweza kupinga maamuzi yako na hakuna wa kuamua Juu/ Zaidi yako.
Kwa unayoyafanya: Kuona kwamba kwa yale unayoyafanya hakuna kama wewe. Hakuna anayeweza kufanya kama wewe.
Kwa unayofanyiwa: Kuona kwamba hakuna anayestahili kufanyiwa kama wewe.
Kwamba Unaweza kufanya chochote: Kudhani kwamba unaweza kufanya chochote kile kwa sababu wewe ni wewe.
Tafakari na ushauri kuhusu UMIMI
Ninapoongelea Umimi siwalengi wenye mamlaka Makubwa ya juu tuu, Nalenga pia mtu mmoja mmoja kwa sababu kila mtu anayo mamlaka na Mwili na Utu wake. Unayo kipawa cha utu wako, uwanaume wako, uwanawake wako, Uzima wako. Vile vile Mamlaka ya Familia yako, jumuiya, ukoo n.k. Unamamlaka ya mwili wako na kwa hiyo kwa mwili huo usiutumie kwa uovu kwa sababu tuu umepewa mwili huo.
Kwa hiyo basi, ninapoongelea UMIMI naanzia chini kabisa kwenye Mamlaka na Mwili wako na Utu wako mpaka kwenye ngazi za jamii Kama Vyeo vya Kijamii na Kiinjili.
Unaweza ukadhani kwamba UMIMI sio makosa lakini makosa yanazaliwa pale unapotenda kwa kufuata umimi wako (Vile ulivyo). Dhambi inakuja pale Kwa sababu ya mamlaka yako unapoamua mambo kwa sababu unajua hakuna wa kukupinga. Kwa sababu ya uwezo wako wa kufanya mambo kufanya vitu kwa ubaya kwa sababu tuu unajua hakuna anayekuzidi/ anayeweza kufanya kama wewe/ anayeweza kukuzuia.
Dhambi inatokana na Kujiona kwako kuwa hakuna anayekuzidi kunakupelekea kushawishika kufanya mambo mengine ili kudhihirisha kuwa hakuna anayekuzidi kweli. Hasa kwa uonevu na ubabe.
UMIMI unaanza kuzaa dhambi pale mtu anapomsahau Mungu wake aliyemuumba na Kumpa huo UMIMI (Kumfanya vile alivyo). Unaposahau kuwa yupo Mungu aliyekupa hayo mamlaka, kipaji, kipawa na cheo ndipo unapoweza kuanza kukosea kwa UMIMI.
Mambo ya kuzingatia kushinda UMIMI
Kushinda UMIMI inahitaji unyenyekevu wa kujitambua kuwa Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo chako Umepewa na Mungu na Unatakiwa Ukitumie kwa Mapenzi ya Mungu.
Ukitaka kuushinda UMIMI unapaswa kutambua kwamba yote yana Mwisho.
Vile vile unatakiwa ujue kuwa Ipo siku utatolea hesabu kwa kile ulichopewa. Ipo siku utaulizwa kwamba Umefanya nini na Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo chako. Ndio maana wenye hekima wanaogopa sana kuwa na Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo kwa sababu wanajua kuwa wanayo kazi kubwa kuliko wale wasiokuwa nacho.
Ukitambua kwamba unawajibika kwa vile ulivyo, basi ujitahidi kutenda kwa kumpendeza Mungu.
KUMBUKA Vile ulivyo inaweza kuwa njia rahisi ya kuufikia Ukamilifu na Utakatifu au inaweza ikawa Mtego kwako kwa kufikia Ukamilifu na Utakatifu. Ni wewe tuu kuamua Unaishije kwa Vile Ulivyo.
3. HASIRA, UKOROFI NA CHUKI
Hasira: Kukasirika haraka kwa kukosa uvumilivu na kutokutambua kuwa unapoishi na binadamu wengine ni lazima/ kawaida kukwazika. Watu hawawezi kufanya yote unayoyataka.
Ukorofi: Kuwa mbabe na kuweka vizuizi na masharti ya kiukorofi, pamoja na kufanya vitendo vya ukorofi na ukaidi kwa walio chini yako na hata walio juu yako.
Chuki: Kuwa na kinyongo na uchungu na watu wengine ambapo matokeo yake ni kufanyiana vitendo vya kikatili huku ukiwaza kuwa ni halali yako.
Tafakari na ushauri kuhusu Hasira, Ukorofi na chuki
Hasira, Ukorofi na chuki ni mambo ambayo mara nyingi yanaweza kuonekana sio dhambi moja kwa moja ila matokeo yake ndio yanaonekana kuwa ni dhambi. Hii ni kwa sababu kwa hali ya kawaida ya binadamu ni kawaida kwa mtu kuwa na Hasira, Ukorofi na chuki lakini vile anavyotenda baada ya kupata hasira au chuki inayopelekea ukorofi ndio inayosababisha mambo haya kuzaa dhambi.
Jambo lililo baya Zaidi ni kwamba dhambi inayotokana na Hasira, Ukorofi na chuki mara nyingi huonekana kama ni halali na haki ya mtu. Kwa Mfano, watu wengi wanaona kuwa ni kawaida kuwa mtu akikukasirisha lazima umfanyizie/ umtendee kitu kibaya. Wengine wanafikiri kuwa mtu anapokukasirisha lazima umuonyeshe ubabe. Na wengine wanaona ni kawaida kabisa kuwa na chuki na kinyongo hasa wanapotendewa visivyo na kuhisi kuwa ni haki yao kuchukia na kuwa na Kinyongo.
Lakini ukweli ni kwamba matendo yote yanayotendwa kwa Hasira, Ukorofi na chuki ni dhambi na makosa mbele ya Mungu. Kushindwa kuzuia Hasira, Ukorofi na chuki ni chanzo kikubwa cha dhambi kwa Wakristu walio wengi hasa Watumishi wa Mungu.
Makosa na dhambi za Hasira, Ukorofi na chuki yanawakoseha Neema za Mungu Watumishi wengi wa Mungu kwa sababu wengi wao hawaoni kama ni dhambi au ni makosa kufanya jambo kwa Hasira, Ukorofi na chuki. Wapo waumini na Watumishi wengi wa Mungu ambao wanaweza kufwatilia kikamilifu matakwa yote ya Imani yao lakini wanalegalega katika Imani yao kwa sababu ya kushindwa kutambua na kujiepusha na makosa na dhambi zitokanazo na Hasira, Ukorofi na chuki.
Mambo ya kuzingatia kushinda Hasira, Ukorofi na chuki
Kushinda Hasira
Ili kushinda hasira ni muhimu kuishi kwa kujua wakati wowote ule yupo mtu anaweza kukukosea.
Ni vizuri kuelewa kua wote wanaokukosea hawakukosei kwa kupenda au kwa kusudi. Ni lazima kutambua Katika maisha kuna mambo mengi yanayoweza yakafanya mtu akukosee au kukukwaza wewe. Huu ndio uhalisia wa Maisha.
Ni vizuri kujua kuwa Hasira ni hali inayoweza kuzimwa ukiamua kuizima na ni hali inayoweza kuwaka sana ukiamua kuiwasha. Sasa ni wewe kuchagua kuizima au kuiwasha.
Muhimu Zaidi kukumbuka ni kwamba Umeitwa Kuishi upendo wa Mungu na wa Jirani kwa maana hii umeitwa kusamehe na kuvumilia wengine huku ukiwaongoza na kuwaelekeza kile kinachotakiwa.
Kushinda Ukorofi
Namna kuu ya kushinda ukorofi ni kuwa mvumilivu. Kuwa mvumilivu na kuweza kuachilia (Kupotezea).
Unaweza kushinda ukorofi kwa Kutambua kuwa sio mara zote ni lazima kushindana na kubishana.
Kushinda Chuki
Kushinda chuki ni ngumu sana hasa unapokuwa tayari na katabia ka kuweka kinyongo au kuona uchungu/ wivu.
Wewe kama Mtumishi wa Mungu unaweza kushinda chuki kwa kujiepusha na tabia ya Kushindana na Kujilinganisha.
Chuki ni tabia au mazoea na kwa sababu hiyo unapotaka kuishinda unatakiwa ujijengee tabia na mazoea ya kinyume chake ambayo ni kujiepusha na mashindano na Kujilinganisha.
Zaidi sana, chuki inaweza kushindwa kwa ukarimu. Unapokua mkarimu unashinda chuki na wivu. Vilevile kwa ukarimu huu unaweza ukazuia chuki ya watu wengine. Utawasaidia wengine wasiwe na chuki na wewe pia, huku na wewe unajizuia na chuki.
MWISHO
Katika mambo yote haya Matatu unaweza ukaona kuwa naongelea Dhambi ya asili ya Binadamu. Dhambi ya Asili ya Binadamu ya Kujiona (PRIDE). Kila binadamu anazaliwa kwa kiasili akiwa na hali ya kujiona (PRIDE). Kila binadamu anazaliwa akiwa anajiona kuwa yeye ni yeye na Hakuna kama yeye.
Hali hii ya kuzaliwa ya kujiona ndio inayopelekea Majivuno, Umimi pamoja na Hasira, Ukorofi na chuki
Kuweza kuushinda kabisa Utu na Ubinadamu wako hapo utakua umeweza kushinda Ile asili yako ya dhambi. Ukiweza kushinda ile asili yako ya dhambi ndio utakuwa umejiepusha na makosa haya.
Tunakosa Utii kwa Mungu tunaposhindwa kupambana na Majivuno, Umimi pamoja na Hasira, Ukorofi na chuki
Mungu ametupa Amri Kuu ya Upendo. Upendo kwake na kwa Binadamu. Lakini amri hii haiwezi kutimizwa kama hatutaweza kushinda kwanza Majivuno, Umimi, Hasira, Ukorofi na Chuki.
Mungu na Akubariki sana kwa Neema zake na akuwezeshe uweze kushinda dhambi na makosa yasiyoonekana kama dhambi, ambayo ndiyo yanayozuia Waumini na watumishi wa Mungu kuufikia Ukamilifu na Utakatifu.