Ujana ni kipindi cha mabadiliko kutoka utotoni kuelekea utu uzima, wakati wa kipindi hiki kijana hupata mabadiliko ya kimwili, kiakili na kimtazamo. Mwili na akili hupevuka. Ni kipindi muhimu cha kuweka msingi wa maisha ya baadaye. Vijana wanakatazwa kujamiiana kwa sababu matatizo mengi yanaweza kutokea kutokana na tendo hilo.
Kwanza kabisa kwa kujihusisha na kitendo cha kujamiiana vijana wanapoteza nguvu na muda ambao wangeweza kutumia kwa shughuli za maendeleo. Kwa mfano, kusoma, kufanya kazi, kushiriki katika shughuli za vikundi katika jamii au kucheza michezo.
Pili, matatizo ya mimba katika umri mdogo ni mengi. Mojawapo ni msichana kufukuzwa shule, au hata jamii kumtenga. Matatizo mengine ni ya kiafya kutokana na mwili wa msichana bado kuwa haujakomaa vyema.
Tatu, vijana wanakuwa bado hawajajiandaa kwa uzazi au kujitegemea. Sababu nyingine ya kuwakataza vijana kujamiiana ni ile ya hatari ya kuambukizana magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na Virusi vya UKIMWI. Magonjwa haya ni mabaya sana yanaweza kusababisha maumivu makali, ugumba au hata kifo.
Unapofikiria sababu zote hizo utaona kwamba kujamiiana katika umri mdogo kunaweza kuleta madhara mengi kwa afya yako na malengo yako maishani. Hivyo basi unapokatazwa kujamiiana ni kwa sababu ya matatizo haya. Hata hivyo, kama kwa vyovyote huwezi kuacha kujamiiana, hakikisha kwamba unajikinga wewe na mpenzi wako kwa kutumia kondomu.
No comments yet. Be the first to share your thoughts!