Updated at: 2024-07-16 11:49:40 (8 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Nini maana ya Kwaresima?
Kwa Kilatini na Kiitaliano neno Kwaresima lilimaanisha “40” yaani siku 40 za kufunga za wiki kati ya Jumatano ya Majivu hadi Jumamosi Kuu. Kwa Kijerumani Kwaresima maana yake “Kipindi cha kufunga.”
Kwaresima ilianzaje?
Kabla ya kuona Kwaresima jinsi ilivyoanza, ni vizuri kuongea kidogo kuhusu Sikukuu ya Pasaka ili tuweze kupata mwanga wa kuelewa mwanzo wa kipindi hiki muhimu cha Kwaresima.
Habari Njema yatuambia kwamba YESU KRISTO alifufuka “Siku ya kwanza ya juma.” “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” (Mt.28:1) Hii ni kwasababu Wakristo walianza kukutana pamoja kwa sikukuu ya ufufuko wa BWANA kila wiki sio Jumamosi kama Wayahudi, bali siku iliyo fuata. “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza -`maneno yake hata usiku wa manane.” (Mdo.20:7). “Siku ya Kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake: ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.” (1Kor.16:2), siku ambayo Warumi waliita “Siku ya Jua”. Mara moja jina hilo lilibadilika na kuwa “Siku ya BWANA”
Kanisa la mwanzoni halikusherehekea sikukuu kama vile Noel, Sikukuu kwa heshima ya Mama Bikira Maria au sikukuu yeyote ile. Kulikuwepo na adhimisho la ufufuko wa BWANA kila wiki na hakuna zaidi.
Miaka mingi ikapita kanisa likiwa katika hali hii. Baadaye kulikuwepo na hitaji la kusherehekea tukio la kiini cha imani yetu kwa namna ya pekee. Wakristo waliona umuhimu wa kuwa na muda kwa sikukuu ya kwanza kati ya sikukuu zao yaani “Jumapili ya Pasaka”, ambayo ilifikiriwa kama “Mama wa Jumapili zote”, “Mama wa skikukuu zote”. Waliiona sikukuu hiyo kama “Malkia wa sikukuu zote, wa Jumapili zote, na kiujumla kama Malkia wa siku zote za mwaka. Tangu mwanzoni mwa karne ya pili, Jumuiya zote za Kikristo walikuwa wanasherehekea sikukuu hii ya Pasaka. Sherehe zilikuwa zinahitimishwa na kusanyiko la sala lililofanyika usiku na kumalizikia na Ekaristi. Ushiriki wa kwenye ibada hiyo, ulichukuliwa kama ni kitu muhimu sana kwa mkristo.
Kuanza kwa Kwaresma
Wote tunafahamu kwamba, ufanisi au mafanikio yoyote ya sikukuu au ya jambo lolote yanategemea sana maandalizi yake. Miaka miambili hivi baada ya KRISTO, Wakristo walitaka kuvuna matunda ya kiroho ya Paska kwa wingi. Ili kufanikisha hili, walianzisha utamaduni wa kuwa na siku tatu kabla ya Pasaka kwa sala, tafakari na kufunga kwa nia ya kuonyesha masikitiko yao juu ya kifo cha YESU KRISTO. Kutokana na ukubwa na umuhimu wa sikukuu hii, mbali ya kuona umuhimu wa maandalizi, walitafuta njia za kuongeza muda wa furaha na utajiri wa kiroho utokanao na Pasaka. Hivyo walianzisha “Wiki Saba,” yaani siku 50 za Pentekoste ambapo walisherehekea na kuzipitisha siku hizo kwa hali ya furaha. Askofu Mt. Ireneus alisema kuwa muda huo wa siku 50 ni kama Sikukuu ya Siku moja yenye umuhimu sawa na Jumapili. Katika kipindi cha siku za Pentekoste, sala zilikuwa zinasaliwa hali wamesimama, kufunga kulikatazwa na sakramenti ya ubatizo ilikuwa ikiadhimishwa. Ni kama vile sikukuu ya Pasaka ilidumu kwa kipindi chote cha siku 50. Miaka 150 ilipita na mwishoni mwa mwaka 350 B.K., Wakristo waliona kama siku tatu hazikutosha kwa maandalizi ya sikukuu kama hii. Hivyo waliongeza hadi kufikia siku 40. Hivi ndivyo Kwaresima ilivyoanza.
Kwa nini siku 40?
Tunaposema kuku wanne au kilo saba za mchele tuna maana kama ilivyo yaani kuku wanne na kilo saba za mchele. Si zaidi au pungufu.
Namba au tarakimu mbalimbali tunazokutana nazo katika Biblia zinaashiria lugha za picha na siyo kuchukulia katika thamani ya kuhesabu. Hivyio basi, tunapokutana na namba kama 40 huenda isimaanishe 40 kama tunavyo hesabu fedha. Kati ya maana nyingi zilizotolewa kwa namba 40, kuna moja yenye maana ya pekee, inamaana ya kipindi cha maandalizi cha kutosha kisichokuwa na muda maalum, kwa tukio kubwa. Kwa mfano , Gharika ilidumu kwa siku 40 usiku na mchana…na ilikuwa ni maandalizi ya ubinadamu mpya; Waisraeli walitumia muda wa miaka 40 jangwani…maandalizi ya kuingia nchi ya ahadi; watu wa Ninawi walifunga na kufanya kitubio siku 40…maandalizi ya kupokea msamaha wa MUNGU; Elia alitembea kwa siku 40 mchana na usiku…kama maandalizi ya kufika mlima wa MUNGU; Musa na YESU walifunga kwa siku 40 mchana na usiku… kama maandalizi kabla ya kuanza utume wao. “Kisha ROHO alimwongoza YESU mpaka jangwani ili ajaribiwe na ibilisi. Akafunga siku arobaini usiku na mchana, na mwishoe akaona njaa” (Mt.4: 1-4)
Natumaini hadi hapo tumeelewa nini maana ya namba 40. Je, ni siku ngapi ambazo zinahitajika kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu kubwa kuliko zote za kikristo? Bila shaka ni 40. (Kuanzia Jumatano ya majivu hadi Jumamosi Kuu ukiondoa Jumapili zote) Siku 40 ni muda wa kutosha wa kufanikisha kitu fulani chema, kizuri na chenye thamani.
Lengo la Kwaresima ni nini?
Lengo kuu la Kwaresima ni kufanya upya maisha yetu ya kiroho na kutufanya kuwa watu ambao MUNGU anataka tuwe yaani ni kipindi chenye kutupatia utakatifu, tukikumbuka kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu kama BABA yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu (Mt. 5:48). Ni kipindi cha kuuvua utu wetu wa kale na kuvaa utu mpya. Kwani tunasoma:- “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unao haribika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa na MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake…Mwibaji asiibe tena…Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema na kufaa…tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.” (Efe.4:22-32.)
Kwaresima kwa hakika ni kipindi pia cha kuachana na matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo;” (Gal.5:19 – 20).
Kwa ufupi Kwaresima ni kipindi cha kuachana na maisha ya dhambi na kurudi kwa MUNGU kwa kuishi maisha yanayompendeza MUNGU kwa njia ya kufanya toba ya kweli isiyo ya mazoea, na malipizi yasiyo ya nje tu, bali hasa mapinduzi ya kiroho. Katika kipindi hiki tunalazima ya kubadili hali yetu ya ndani. Badala ya kujitafuta wenyewe na kufuata mapenzi yetu, inatupasa sisi kumwelekea MUNGU na kuyatimiza mapenzi yake katika mawazo, maneno na matendo yetu.
Nguzo tatu kuu za Kwaresima ni:
i. Sala.
“Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani. Usali mbele ya BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakujazi.” (Mt. 6:6)
Kupata muda wa sala pamoja na MUNGU. Sio tu kunena maneno ya sala fulani, lakini pia kumsikiliza MUNGU akizungumza mioyoni mwetu. Kumuomba MUNGU nguvu ya kubadilika, yaani uongofu wa kweli. Ndiyo maana tunaambiwa. “Tubuni na kuiamini Injili”. Hayo ndiyo MUNGU aombayo kwetu wakati wa Kwaresima. MUNGU anatuita kutoka kwa dhambi, na tuupokee ujumbe wake kwetu – Injili, na kuwa waamninfu kuishi kadiri ya Injili. Ni wakati pia wa kuhudhuria misa mara kwa mara kwa ibada na uchaji, kuhudhuria ibada mbalimbali, kama vile Baraka ya Sakramenti Kuu, Kuabudu Ekaristi Takatifu, kusoma Neno la MUNGU na kuliishi baada ya kuyatafakari maneno hayo ya MUNGU ambayo ndiyo sauti yake MUNGU na kutumia muda wetu kwa mambo ya ki-MUNGU yaliyo matakatifu.
ii. Kufunga.
“Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso wako ili usionekane na watu ukifunga, ila na BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakutuza.” (Mt. 6:17-18). Kufunga sio tu kujinyima kutokunywa pombe, kutokula chakula, kutovuta sigara n.k. Kifupi ni kwamba kufunga kuondokana na ubinafsi wetu na kuwafikiria na kuwasaidia wenye shida. Uovu hauwezi kushindwa bila kujitoa nafsi na bila kutoa na kuwapa wahitaji vile tuvipendavyo. MUNGU hapendezwi na kufunga tu, bali upendo kwa wanaoteseka utusukume na kufunga tupendavyo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Hivyo kuna mahusiano makubwa sana kati ya kufunga na ukarimu. Kufunga lazima kuendane na ukarimu. Kufunga bila ukarimu huo ni mfungo tasa.
iii. Kutoa Sadaka.
“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe nao. Bali wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa kuume; na BABA yako aonaye kwa siri atakujazi.” (Mt. 6:1) Hayo yanamaanisha kwamba usidai shukurani wala malipo kwa wema wowote uwatendeao jirani zako kwa sadaka yako. Malipo utakayopata uyatazamie tu kutoka kwa BABA yako wa mbinguni. Kutoa tunachojinyima kwa kumsaidia KRISTO anayeteseka kwa wenzetu. Kushirikiana na wengine tulivyo navyo kama vile fedha, nguo, chakula, ama kuwakaribisha wahitaji nyumbani.
Hivyo basi, Mazoezi tunayofanya katika kipindi cha Kwaresima kama kusali zaidi, kusikiliza au kusoma Neno la MUNGU, kutenda matendo ya huruma kwa wahitaji, kufunga chakula na kujihinisha kinywaji pamoja na kuzuia tamaa potovu za mwili wetu, yawe na kusudi la kuibadili hali yetu, kutufanya kuwa na upendo zaidi na huruma kwa wenzetu na kutufanya tuweze kuunganika zaidi na KRISTO MFUFUKA. Tumvue mtu wa zamani katika nafsi zetu na tumvae mtu mpya, yaani KRISTO Mfufuka.
Nini makusudi ya kufunga?
YESU alifunga ili awape wanadamu mfano au kielelezo halisi na sahihi cha kuiga, na apate kuokoa roho zetu. Watu wawe na namna bora ya kufanya malipizi, kuuadibisha na kuutumikisha mwili na tamaa kwa kuwa anatenda dhambi.
Nani anapaswa kufunga?
Inatubidi tujiangalie sana kwani miili yetu ni midhaifu na myepesi kwa kutenda dhambi na kuipeleka roho motoni. Tusiiendekeze miili yetu, bali tuitawale kwa kufuata maadili ya kimungu na kuinyima madai yake, ambayo ni kishawishi kinachotupeleka upotevuni. Tunapoamua kufuata njia hii, hakika, KRISTO atatuimarisha na kutuongoza kwenye uzima wa milele; na kutupa neema ya kupambanua mema na dhambi, huku tukielekea uzimani. Mdomo unao nena dhambi, na mwili unaotenda dhambi, sherti vyote vitende pia mema, siyo dhambi.
Mtu asiyetenda dhambi hana haja ya kufunga. Lakini hakuna mtu anyefikia utu uzima ambaye hatendi dhambi machoni pa MUNGU hata Wacha MUNGU wana dosari. Kwa hiyo, kila mtu afunge kufidia dhambi zake. Tusipofunga kuna hatari kubwa ya kuungua moto. Ni vizuri waamini wote wafunge ili kulipia fidia ya dhambi zinazotendwa. Tumwabudu KRISTO kwa unyofu na unyenyekevu, ili kwa huruma yake kuu atusamehe dhambi zetu na adhabu tunazostahili.